Ni Aprili nyingine. Kumbukumbu za siku ile ya majonzi zinabisha hodi tena, zikijitokeza kwa ujasiri mithili ya jua la asubuhi lisilozuilika. Tarehe kumi Aprili mwaka wa elfu mbili ishirini haikuwahi kuwa siku ya kawaida. Siku hiyo, fasihi ya Kiswahili ilimpoteza mwanawe kipenzi, mtafiti wa nafsi za wahusika na msanii wa maneno, Profesa Ken Walibora. Na leo, miaka mitano baada ya mwanga huo kuzimwa na kiza cha ajabu, bado mwanga wake haujapotea kabisa. Miale yake inaendelea kuwaka, ikiangaza matumaini katika mioyo ya wasomaji, waandishi na wanazuoni.
Ken Walibora hakuwa mwandishi tu. Alikuwa msimulizi wa roho, mvuviaji wa fikra, mpambanaji wa lugha. Aliweza kuibua hisia nzito kwa maneno mepesi, kuumba wahusika wa kubebwa moyoni na kutumia Kiswahili kama chombo cha kutibu, kufundisha na kuhamasisha. Kupitia kazi kama vile Siku Njema, Kidagaa Kimemwozea na Ndoto ya Amerika, alitusawiri jamii inayotapatapa kutafuta uhalisia wake, jamii iliyojaa ndoto, vizingiti na matumaini yanayong’aa katikati ya majonzi.
Jina lake halisi lilikuwa Ken Walibora Waliaula. Msomi huyu mwenye shahada ya uzamifu alizivuka bahari za maarifa, akafundisha katika Chuo Kikuu cha Ohio State nchini Marekani kabla ya kurejea nyumbani kama mwana wa ardhi aliyetamani kuirudishia jamii yake alichopata ughaibuni. Alikuwa kiungo cha thamani kati ya darasa na mtaa, akiandika kwa ajili ya mwanafunzi, lakini pia kwa ajili ya mama mboga na kijana wa mtaa wa Majengo.
Mimi ni kati ya walioguswa na kalamu yake. Siku Njema ilikuwa mlango wangu wa kwanza kuelekea kwenye hekalu la fasihi ya Kiswahili. Nilikutana nayo nikiwa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Shing’oto iliyoko Navakholo katika Kaunti ya Kakamega. Nilikuwa bado mchanga, nikiibua ari ya lugha, na hapo ndipo nilikutana na Misanifu Kombo, kijana aliyejua uchungu wa kutafuta mzizi wa jina lake na fahari ya kuwa mtu kamili. Nilijitambua katika huzuni na matumaini yake, nikashikwa na mshangao wa lugha iliyosokotwa kwa ustadi wa kipekee, ikikonga roho yangu kama muziki wa taarabu kwenye jioni tulivu ya pwani.

Kalamu ya Walibora ilinivutia kwa nguvu ya ajabu. Kwa msukumo wa kazi zake, nilianza kuchochewa na hamu ya kuandika kwa Kiswahili, nikijifunza kutoka kwa uandishi wake uliojaa upekee wa kifasihi. Nikatumia msamiati wa kina, nikacheza na methali, nikasuka insha zilizozua mshangao. Lakini mwalimu wangu wa Kiswahili, Bwana Francis Wanyama, hakuweza kufuatilia haraka ya ndimi yangu. Alinipunguza kasi kwa ukarimu mkali, akaniambia kwa upole, “Punguza mzigo, wanaoandamana nawe hawajafika hapo.” Alinipa alama ndogo, akavunja moyo wangu kama kioo kilichoangushwa ghafla. Nilitoweka kwenye uwanja wa insha kwa muda.
Lakini kama Walibora alivyoandika katika Siku Njema, “Nilikuwa nimepigwa na hali yenyewe.” Baadaye, mwalimu huyo alikuja kunielewa, akaniinua tena. Akaanza kuniongoza taratibu, akinifundisha kuwa fasihi si mbio za kufika haraka bali ni safari ya uvumilivu na mazoea ya roho. Leo hii, ninapotazama nyuma, ninamshukuru kwa fimbo yake ya kiwalimu iliyojaa busara na huruma.
Miaka michache baadaye, nilichapisha makala yangu ya kwanza kwa Kiingereza katika mtandao wa gazeti la The Standard. Nikaanza kuamini kuwa uandishi haukuwa ndoto ya mchana. Ndipo nikarudi tena kwa Walibora, rafiki wa fasihi yangu ya awali. Nikaisoma Siku Njema kwa macho ya mtu mzima, na mara hii, nikaitazama kama ramani ya kujielewa na mwongozo wa kuchonga sauti yangu ya uandishi. Nilitamani kuchangia katika gazeti la Taifa Leo, lakini woga na shaka vilinizuia. Ndoto hiyo ililala usingizi mzito, lakini haikufa.
Leo hii, ninaposoma tena kurasa zake, najikuta nikitafakari kwa kina. Ni kwa kiasi gani nimenolewa na maandishi haya? Ni kwa jinsi gani kalamu ya Walibora imekuwa kama kisu cha kutakasa nafsi yangu ya kisanaa? Siku Njema ni zaidi ya hadithi, ni urithi, ni ibada, ni kioo cha jamii kilichoshikwa kwa unyenyekevu wa kipekee.
Ken Walibora alithibitisha kuwa lugha ni mwili wenye roho. Na hata sasa, sauti yake inasikika, si kwa redio wala televisheni, bali kupitia kurasa zake zenye pumzi ya milele. Na sisi, wanafunzi wa kalamu yake, tunao wajibu wa kuendeleza mwako huo, kuandika, kusimulia na kutafsiri ndoto zetu kupitia Kiswahili.
Nguli huondoka, lakini sauti zao huzama ndani ya nafsi za waliosoma maandishi yao. Walibora hayupo nasi kimwili, lakini kila neno lake bado linaishi. Kila ukurasa wake bado unavuta pumzi. Na sisi tunaobeba urithi wake, lazima tuiimbe tena ile kauli ya mwisho ya Siku Njema:
Redio hutangaza: Siku njema
Nasi twaitikia, maneno yakielea
Siku njema, siku njema
Lakini, kweli ni siku njema
Naam, ni siku njema. Kwa sababu urithi wa Ken Walibora bado waimba.
Facebook Comments