Wababe wa KSSSA Kakamega Watinga Nusu Fainali

Mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Shule za Sekondari (KSSSA) katika Kaunti ya Kakamega yameingia hatua ya nusu fainali huku timu mahiri zikidhihirisha ubabe wao uwanjani. Wachezaji kutoka shule mbalimbali wameonyesha kiwango cha juu cha mchezo, wakisajili ushindi wa kuvutia na kuwapagawisha mashabiki waliofurika viwanjani.

Katika kipute cha wasichana, Butere Girls waliendeleza ubabe wao kwa kuwalaza Ahong’injo mabao 2-0. Kimang’eti Girls walitinga nusu fainali baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Kilimo kisha kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-3. Archbishop Njenga waliwacharaza Sivilie mabao 3-0, huku Mwira Girls wakitoka kifua mbele kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Musoli.

Kwa upande wa wavulana, Kakamega High maarufu kama Green Commandos, walionesha hadhi yao kwa kuwazima Muslim Boys 2-0. Musingu High waliwaangusha Shanderema Boys kwa mabao 3-1, huku Munyuki wakisajili ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Shamberere kufuatia sare ya 1-1. Mchuano kati ya Butere Boys na St. Peter’s Mumias uliahirishwa hadi kesho asubuhi kutokana na giza kuingia kabla ya kupigwa mikwaju ya penalti.

Nusu fainali zimepangwa kuchezwa Juni 21, 2025 katika viwanja vya Mumias Central, Muslim Boys Grounds na Mumias Complex, zikifuatwa na fainali jioni hiyo katika uwanja wa Mumias Sports Complex.

Maafisa wa michezo, wazazi, walimu, na mashabiki wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono vipaji vinavyochipuka. Kaunti ya Kakamega inaendelea kudhihirisha kuwa kitovu cha michezo na ukuzaji wa talanta nchini Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki.

Baada ya fainali za kaunti, timu zitakazofuzu zitawakilisha Kakamega kwenye mashindano ya Ukanda wa Magharibi kabla ya kuelekea kwa fainali za kitaifa na za Afrika Mashariki (FEASSSA) mwezi Agosti.

Kaunti ya Kakamega itakuwa mwenyeji wa mashindano ya FEASSSA katika uga wa kimataifa wa Bukhungu, ambao kwa sasa unakarabatiwa kufuatia agizo la Gavana Fernandes Barasa, kama sehemu ya maandalizi ya hafla hiyo ya hadhi ya juu.

Facebook Comments

By Dennis Weche

Dennis Weche is a seasoned journalist and writer who explores Kenya’s literary landscape with a critical and thoughtful eye. He advocates for the recognition of African authors and the preservation of indigenous languages in contemporary storytelling.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *